Jumatatu , 28th Jul , 2014

Serikali ya Tanzania imesema upo uwezekano wa kuondoa tatizo la ajira nchini kupitia kilimo ambapo kuna asilimia kubwa ya mapato yatokanayo na sekta hiyo hivyo kutengeneza ajira kwa vijana na wastaafu.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Ushirika Dk. Yamungu Kayandabila wakati akiongea na East Africa Radio ambapo amewataka vijana wakiwemo wasomi wajiingize katika shughuli za kilimo ili kupunguza lawama za ukosefu wa ajira.

Naye Victor Temba ambaye ni mhitimu wa chuo kikuu anayejishughulisha na kilimo cha mbogamboga na matunda amesema hakuna msaada wa kifedha na mbinu za kilimo kutoka serikalini na kuongeza kuwa wanaofaidi na misaada inayohusu kilimo ni wakulima wakubwa na si wakulima wadogo kama yeye.

Wakati huo huo, Chama cha kutetea abiria Tanzania (CHAKUA) kimeilalamikia mamlaka ya udhibiti wa usafirishaji wa nchi kavu na majini (SUMATRA) kwa kukwamisha uanzishwaji wa mtandao wa mfumo wa upatikanaji wa tiketi za mabasi yaendayo mikoani kwa njia ya simu.

Akiongea jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Bodi ya CHAKUA Bw Modest Mfilinge amefafanua kuhusu utaratibu wa ukataji wa tiketi kwa njia ya mtandao kuwa utasaidia kuondoa kero ya abiria kupandishiwa nauli kipindi cha sikukuu na pale shule zinapofungwa au kufunguliwa.

Kwa mujibu wa Mfilinge, wadau wa usafirishaji walikutana na SUMATRA ili kupitisha azimio la kuwepo kwa mfumo huo lakini ni miezi mitatu imepita na SUMATRA hawajatoa tangazo rasmi la kuanzishwa kwa mtandao huo.