Jumanne , 24th Jun , 2014

Wizara ya afya na ustawi wa jamii nchini Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa za kuadimika kwa dawa za kufubaza makali ya ukimwi za ARV kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni.

Msemaji wa wizara ya afya na ustawi wa jamii Nsachris Mwamwaja (katikati) akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari MAELEZO hivi karibuni.

Taarifa ya wizara hiyo iliyosainiwa na msemaji wake Bw. Nsachris Mwamwaja imesema taarifa za kuadimika kwa dawa hizo hazina ukweli wowote kwani nchi kwa sasa ina akiba ya kutosha ya dawa hizo.

Kwa mujibu wa Mwamwaja, wizara ya afya na ustawi wa jamiii imekuwa ikiweka kipaumbele kuhakikisha upatikanaji wa dawa hizo ni wa kuridhisha sambamba na kuhakikisha kuwa wagonjwa wanapatiwa dawa hizo bila malipo yoyote.

Aidha Mwamwaja amefafanua kuwa suala la upatikanaji wa dawa za ARV ni la umuhimu mkubwa kwa wizara ya afya na ustawi wa jamii, hasa ikizingatiwa mahitaji ya dawa hizo katika kuimarisha afya za watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.