
Taarifa kutoka kwa kocha mkuu wa timu ya Kilimanjaro Stars Ammy Ninje amesema Mbaraka Yusuph amepona lakini bado hajawa sawa kiasi cha kucheza mchezo wa kesho dhidi ya Rwanda.
Kikosi cha Kilimanjaro Stars kimefanya mazoezi ya mwisho jioni hii kwenye uwanja wa Machakos Academy licha ya mvua zinazoendelea kunyesha katika County ya Machakos.
Mchezo huo wa kundi A utachezwa saa 8 mchana kwenye uwanja wa Kenyatta, Machakos ambapo una umuhimu mkubwa kwa Kilimanjaro Stars katika harakati zake za kuitafuta tiketi ya kucheza hatua ya nusu fainali.
Kilimanjaro Stars ina pointi moja mpaka sasa baada ya kutoka sare na Libya kwenye mchezo wa kwanza kabla ya kufungwa na Zanzibar Heroes kwenye mchezo wake wa pili. Kundi A linaongozwa na Zanzibar wenye pointi sita wakifuatiwa na wenyeji Kenya wenye pointi nne.