Ijumaa , 2nd Mei , 2025

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya, limekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni zinazodai Askari Polisi wamehusika na tukio la kuvamia na kumjeruhi Mpaluka Said Nyagali maarufu kama Mdude Nyagali na kisha kutoweka naye.

Mdude Nyagali

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 2, 2025, limesema kwamba linaendelea na ufuatiliaji ili kumpata mhanga na kuwabaini waliohusika katika tukio hilo kwa hatua zaidi za kisheria.

"Mnamo Mei 02, 2025 majira ya asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipokea taarifa kutoka kwa Sije Mbugi Emmanuel (31) mkazi wa Iwambi ambaye ni mke wa Mpaluka Said Nyagali @ Mdude kuwa mnamo Mei 02, 2025 majira ya saa 8:00 usiku wakiwa wamelala mtaa wa Ivanga, Kata ya Iwambi Jijini Mbeya kuwa watu wasiofahamika waliwavamia baada ya kuvunja mlango na kuingia ndani na kisha kumjeruhi Mpaluka Said Nyagali @ Mdude sehemu mbalimbali za mwili wake. Aidha, watu hao baada ya tukio hilo walifanikiwa kutoweka na mhanga na kwenda naye kusikojulikana," imeeleza taarifa ya Polisi Mbeya

Aidha Jeshi hilo limetoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo Mdude Nyagali azitoe ili kufanikisha kumpata pamoja na taarifa za watu waliohusika katika tukio hili ili waweze kukamatwa.