Jumapili , 23rd Nov , 2025

Waliofariki katika ajali hiyo ni wanaume watatu na wanawake wawili, huku majeruhi akiwa ni mwanamke ambao wote walikuwa ni abiria katika gari ndogo.

Watu watano wamefariki dunia huku mmoja akijeruhiwa baada ya magari mawili kugongana leo huko katika maeneo ya Mbuyuni, wilaya ya monduli Mkoani Arusha.

Taarifa hiyo imetolewa leo Novemba 23, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema ajali hiyo imetokea leo muda wa saa saba mchana.

SACP Masejo amebainisha kuwa ajali hiyo imehusisha basi la abiria lenye namba za usajili T. 922 DZQ aina ya Yutong likitokea Dodoma kwenda Arusha na kugongana na gari ndogo lenye namba za usajili T. 705 DFP aina ya Mark X likitokea Arusha.

Waliofariki katika ajali hiyo ni wanaume watatu na wanawake wawili, huku majeruhi akiwa ni mwanamke ambao wote walikuwa ni abiria katika gari ndogo.

Aidha, Jeshi hilo limesema linaendelea kufanya Uchunguzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo, ambapo majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Jeshi Monduli kwa ajili ya matibabu, na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Makuyuni.

Kufuatia ajali hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limetoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari na kufuata sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani wakati wote waendeshapo vyombo vya moto ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea.