Jumapili , 4th Mei , 2025

Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa, linachunguza tuhuma za askari wawili kuhusika kwenye tukio la kujeruhiwa na kupotea kwa kada wa CHADEMA Mdude Nyagali.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania

"Jeshi la Polisi linafuatilia kwa karibu tuhuma zilizotolewa na mwananchi mmoja ambaye jina lake linaendelea kufuatiliwa akiwatuhumu askari wawili kupitia mitandao ya kijamii kuwa walimfuata na kumtaka afanye nao kazi ya kijajusi pamoja na kumuahidi kumpatia fedha,"

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini David Misime, imeeleza kuwa kufuatia taarifa hiyo, Jeshi la Polisi kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai limeunda kikosi kazi ambacho tayari kimeshafika mkoani Mbeya kwa ajili ya uchunguzi juu ya suala hilo. 

Wakati uchunguzi juu ya suala hilo ukiendelea, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi, yeyote mwenye taarifa zitakazosaidia kubaini ukweli juu ya suala hili atoe ushirikiano kwa kutoa taarifa hizo kwa Jeshi la Polisi.