Jumatatu , 8th Mei , 2017

Msanii wa bongo fleva mwenye 'hit song' ya 'Acha niende' Baraka Da Prince amefunguka mazito kwa kuwachana mashabiki wa kusema hajawahi pata kuona watu wajuaji na wenye chuki kama watanzania kwa kujifanya kila kitu wanajua wao kuliko wahusika wenyewe.

Msanii wa bongo fleva, Baraka Da Prince

Baraka amesema hayo kupitia ukurasa wake wa istagramu baada ya baadhi ya mashabiki kuanza kuiponda kazi mpya ya iliyotolewa na msanii Darasa iliyopewa jina la 'Hasara roho' kwa kudai wimbo huo kuwa ni mbaya wala haufanani na muimbaji husika

"Tangu nazaliwa sijapata kuona nchi yenye wajuaji wengi kama Tanzania.. Tangu nazaliwa sijawahi kupata kuona nchi yenye binadamu wenye chuki baada ya  kuona mtu kafanikiwa kama Tanzania, siku hizi mashabiki wamekuwa walimu wa mashairi na wamekuwa wajuaji kuliko hata sisi tunaoimba muziki....Darasa katoa wimbo wake mpya ni mkali sana sio 'audio' tu hadi 'video' ...Ujue muziki sio kitu kirahisi kama watu wengi humu ndani mnavyodhania na siyo lazima kila kitu kiwe sawa au mapokezi kufanana na kilichopita nyuma". Alisema Baraka

Aidha, msanii huyo aliendelea kwa kusema kuwa hakuna jambo baya duniani kama mtu kujitoa kuamua kufanya kitu fulani halafu wanatokea baadhi ya watu kuanza kukuponda ulichokifanya.

"Hakuna kitu kinaboa duniani kama mtu unapoteza muda wako na nguvu nyingi kuwekeza katika kazi yako au kupigania mafaniko yako halafu kinakuja kijimtu sijui hata kimetokea wapi kinaanza kuponda kile kitu ulichopoteza muda, nguvu nyingi na pesa..Nyie watu wajuaji kinoma, tungeni zenu nzuri na 'video' zenu nzuri tuzione..Hao hao kesho ndiyo utawasikia wakiimba kama wimbo wa taifa". Alisisitiza Baraka