Alhamisi , 3rd Nov , 2016

Serikali ya Japani imeahidi kutoa kiasi cha dola 126,726, ambazo ni sawa na shilingi Milioni 268 za Tanzania kwa ajili ya kufanikisha Ujenzi wa Chumba cha upasuaji katika kituo cha Afya Nkoma kilichopo Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu

Masaharu Yoshida, Balozi Japan nchini

 

Balozi Japan nchini, Masaharu Yoshida Amesema Japan imekuwa ikifadhili miradi midogomidogo kwa ajili ya maendeleo ya jamii kupitia mfuko maalum, pamoja na kushirikiana na nchi za Afrika Ikiwamo Tanzania katika kuendeleza sekta ya afya.

"Katika Wilaya ya Itilima, huko mkoani Simiyu kuna vituo vitatu tuu vya afya huku kukiwa na uhaba wa chumba cha upasuaji, huku ripoti ya mwaka 2015 inaonyesha wanawake 13 hupoteza maisha wakati wa kujifungua kwani nilazima wasafiri kilometa 40 kufika hosptali ya Bariadi ambako kuna chumba cha upasuaji hivyo nilazima tulishugulikie kuokoa maisha ya mama na mtoto"

Mkurugenzi wa wilaya Itilima, alisema mradi huo utasaidia kupunguza tatizo la huduma za upasuaji kwa kinamama 3,000 hadi 4,000 kati ya wajawawazito 13,000 ambao hujifungua katika kituo hicho kwa mwaka.

Alisema wilaya hiyo, ina vituo vitatu vya afya ikiwamo kituo cha Nkoma kilichopatiwa msaada huo na kwamba ujenzi utakapokamilika utawapunguzia wagonjwa waliokuwa wanatembea umbali wa kilometa 40 kufuata huduma hadi hospitali ya wilaya ya Bariadi.

Aidha, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation, Dk. Ellen Senkoro amesema taasisi hiyo inatekeleza miradi ya kujenga vyumba vya upasuaji katika vituo vilivyopo katika mikoa saba nchini, ikiwamo Rukwa, Kagera, Simiyu na Shinyanga kwa lengo la kufikia asilimia 50 ya vituo vya Afya vinakuwa na vyumba vya upasuaji.