Ijumaa , 22nd Apr , 2016

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametetea maamuzi yake ya kuwawajibisha watumishi wa umma hadharani na kusema kuwa kwa kuwa walitangazwa hadharana basi hakuna budi kuwawajibisha hadharani pia.

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

Rais Dkt. Magufuli amesema hayo jana Ikulu, Jijini Dar es Salaam alipokutana na Wenyeviti na Makatibu wa CCM ,wilaya na mikoa yote nchini na kusema kuwa anawashangaa watu wanaowatetea watendaji hao waliokuwa wakiwaibia Watanzania hadharani.

Akitumia msemo wake maarufu wa “Kutumbua Majipu” rais Dkt. Magufuli amesema wanaosema hakuna haki za binadamu kwa mtindo wa wajibishaji huo na kuhoji mbona wakati wanawaibia wananchi masikini hawakujitokeza kuwatetea kuhusu haki zao zinavyopotea.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa kwa mamlaka aliyonayo ya kuwatangaza dharani na kufurahia basi hakuna budi kuwatumbua hadharani kama alivyowatangaza huku akisisitiza mateso waliyowapa wananchi masikini basi hakuna budi na wao kuyapata.

Katika hatua nyingine rais Dkt. Magufuli amewataka vingozi hao wa CCM kusahau yaliyopita wakati wa uchaguzi na kushikamana kwa pamoja katika kusonga mbele kwa maendeleo ya wananchi na chama chao kwa ujumla.

Kwa upande wake Makamu wa rais wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu, ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi hao wa CCM, kuwaunga mkono kwa jitihada wanazozifanya ili kuwaletea maendeleo wanayoyahitaji.