Jumanne , 11th Nov , 2025

Rapa maarufu wa Marekani Lil Uzi Vert ameshtakiwa na aliyekuwa msaidizi wake binafsi, ambaye anadai alipata msongo wa mawazo na mateso ya kihisia alipokuwa akifanya kazi na msanii huyo katika moja ya ziara zake.

Kwa mujibu wa taarifa za kesi hiyo, mwanamke huyo anadai alikumbana na kauli chafu, mazingira ya kazi yasiyo rafiki, na hata vitendo vya kingono visivyofaa kutoka kwa Uzi.

 

Inadaiwa kuwa alipewa kazi ya kuwa msaidizi wa Uzi mwaka 2022, baada ya msanii huyo kuvutiwa na jinsi alivyokuwa akihudumia wateja alipokuwa akifanya kazi katika duka la Balenciaga huko Los Angeles.

 

Hata hivyo, baada ya kuanza kazi, anadai alianza kukumbana na mazingira yenye shinikizo kubwa, unyanyasaji wa maneno, na uhasama kazini. Aidha, anasema baadhi ya maafisa wa kampuni ya usimamizi wa Uzi, Roc Nation, walihusika au walifumbia macho matendo hayo.

 

Kwa sasa, mwanamke huyo amefungua kesi mahakamani akitaka fidia na haki kwa kile anachokiita unyanyasaji wa kimwili, kihisia na wa kingono alioupitia akiwa kazini kwa Lil Uzi Vert.