Mtuhumiwa Mathias Fabiani John, mwenye umri wa miaka 25, mkazi wa Kata ya Shangani amefikishwa Mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Juma Samli Napone (42), fundi ujenzi na mkazi wa mtaa wa Indiani, Kata ya Shangani, Wilaya ya Mtwara.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara iliyotolewa leo Disemba 31 imeeleza kuwa Mathias amefikishwa mahakamani jana Disemba30, 2025.
Imeelezwa kuwa mnamo Disemba 14, 2025 mtuhumiwa alimkamata marehemu na kwenda naye katika pori la mikoko ambalo lipo katika fukwe za Kata ya Shangani, na ilipofika Disemba 17,2025 majira ya saa sita usiku mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa umeanza kuharibika.
“Awali, mtuhumiwa alimtuhumu marehemu kwa kosa la kuiba pikipiki yake, hata hivyo tukio la kuibiwa kwa pikipiki hiyo halikuripotiwa katika kituo chochote cha Polisi”, taarifa ya Polisi imeeleza.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limetoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi badala yake kutumia njia sahihi katika kutatua changamoto zao, ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi au mamlaka zinazotambulika kisheria ili kumaliza tofauti zao na kubainisha kuwa halitakuwa na muhali kwa yeyote atakayebainika kujichukulia sheria mkononi.
