Jumatatu , 11th Apr , 2016

Klabu ya soka ya Simba imeshindwa kuweka hai matumaini yao yakurejea katika michuano ya vilabu barani Afrika mara baada ya kupoteza nafasi ya kucheza kombe la shirikisho kwa kutolewa katika kombe la shirikisho Tanzania robo hatua ya robo fainali

Wachezaji wa Coastal Union wakishangilia moja ya magoli yao mawili waliyoifunga Simba katika mchezo wa robo fainali ya TFF- FA.

Ndoto za Simba SC kurejea kwenye michuano ya vilabu barani Afrika mwakani zimeyeyuka kwa asilimia hamsini hii leo, baada ya kutolewa na Coastal Union katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la FA.

Hali hiyo ni baada ya kufungwa mabao 2-1 na Coastal katika mchezo mkali uliochukua nafasi katika uwanja wa Taifa, Dar es salaam, ambapo mabao yote ya Wagosi wa Kaya yamefungwa na mshambuliaji kutoka Cameroon Youssouf Sabo aliyewahi kufanya majaribio Yanga, yote kwa mipira ya adhabu moja ikiwa ni Free Kick na la pili kwa Penati

Sabo, aliyetokea Cotton Sport ya Cameroon, alianza kuifungia Coastal Union dakika ya 19 kwa shuti la mpira wa adhabu umbali wa mita zaidi ya 20 na kutinga nyavuni moja kwa moja mpira ukimpita kipa Muivory Coast, Vincent Agban.

Kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Hamisi Kiiza akatokea benchi kipindi cha pili na kwenda kuisawazishia Simba bao hilo.

Ilimchukua dakika mbili tu uwanjani Kiiza kuisawazishia Simba baada ya kuingia dakika ya 47 kuchukua nafasi ya kiungo wa Zimbabwe, Justice Majabvi.

Hata hivyo, Sabo tena akaifungia Coastal bao la ushindi kwa penalti dakika ya 85, kufuatia beki Novaty Lufunga kumuangusha kwenye boksi mshambuliaji Ally Ahmed ‘Shiboli’.

Mwamuzi Alex Mahagi wa Mwanza pamoja na kutenga tuta akamtoa kwa kadi nyekundu Lufunga na kuidhoofisha kabisa Simba.

Kwa ushindi huo, Coastal inaungana na Azam FC, Mwadui FC, na Yanga SC kukata tiketi ya kucheza Nusu Fainali ambayo droo yake inatarajiwa kufanyika kesho April 12.

Katika michezo mingine ya robo fainali za michuano hiyo iliyoanza mwishoni mwa mwaka jana kwa kushirikisha timu 64, Azam FC iliitoa Prisons kwa kuifunga 3-1, Mwadui FC iliitoa Geita Gold kwa kufunga 3-0 na Yanga SC iliwafunga Ndanda FC 2-1.