Jumamosi , 19th Dec , 2015

Vigogo wa soka nchini Tanzania wekundu wa Msimbazi Simba na mahasimu wao Yanga hii leo wameshuka dimbani katika miji tofauti katika moja ya michezo ya ligi kuu bara wakisaka pointi tatu muhimu.

Kikosi cha timu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

Mabingwa wa kombe la mapinduzi ya Zanzibar timu ya soka ya Simba hii leo wakiwa ugenini jijini Mwanza wameshindwa kukata kiu ya mashabiki wao mara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo mkali ambao ulifanyika katika uwanja wa CCM Kirumba ambao ulikuwa ukiteleza muda wote kutokana na kujaa maji baada ya mji wa mwanza kugubikwa na mvua kubwa.

Katika mchezo huo mkali wekundu wa Msimbazi Simba walianza kwa kasi kubwa baada ya kutawala mchezo huo katika dakika 20 za mwanzo huku wakilishambulia lango la Toto Africans mara kwa mara na kunako dakika ya 22, Danny Lyanga anafanikiwa kufunga bao safi kabisa nje ya 18, baada ya kuona kipa ametoka nakupiga mpira wa juu uliojaa wavuni, moja kwa moja.

Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao moja na kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa huku Simba wakikosa magoli kadhaa kupitia kwa washambuliaji wake kama Ibrahim Hajib na Mkenya Raphael Paul Kiongera ambaye alikuwa akichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza akirejea baada ya kutolewa kwa mkopo kwenda timu ya KCB.

Toto Africans ilipata bao al kusawazisha katika dakika za majeruhi kabisa kipindi cha pili Dk 90+2 kupitia kwa mshambuliaji wake Everist Benard akifunga goli zuri kwa kichwa baada ya beki Hassan Isihaka kushindwa kuruka juu na kupiga kichwa kuokoa, mpira ambao ukamkuta mfungaji.

Katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam wenyeji Yanga hii leo wamewapigisha kwata wapiga debe wa Shinyanga timu ya Stand United baada ya kuipa kichapo cha bao 4-0 kwa magoli ya washambuliaji mrundi Amis Tambwe ambaye alipiga magoli matatu [Hat Trick] huku la nne likifungwa na mzimbabwe Thaban Kamusoko.

Matokeo mengine ni huko katika dimba la Kaitba mjini Bukoba mkoani Kagera wenyeji wakata miwa wa Kagera Sukari wameichapa timu ya African Sports kwa jumla ya bao 1-0 goli pekee likifungwa na beki asiyekata tamaa Salum Kanoni.

Katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya wenyeji wa uwanja huo maafande wa Tanzania Prison wamebanwa mbavu na wakata miwa wa Manungu mkoani Morogoro timu ya Mtibwa Sukari baada ya kutoka suluhu [0-0].

Kwa matokeo hayo Yanga imeendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo kwa kujikusanyia alama 30 nne mbele ya Azam FC yenye alama 26 na michezo miwili nyuma, huku Mtibwa Sukari wao wakikamata nafasi ya tatu kwa alama 24 wakifuatiwa na Simba yenye alama 23.