Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Charles Mkumbo.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa jeshi la polisi mkoani humo, Charles Mkumbo, wakati akifungua mafunzo kwa maofisa wa polisi mkoani humo yaliyokuwa na lengo la kuwawezesha maofisa hao kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu katika nchi inayofuata misingi ya utawala wa demokrasia hasa wakati huu ambao taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Amesema tayari askari polisi wamepewa mafunzo mbalimbali ya namna ya kusimamia uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa polisi kwa kulinda amani siku hiyo.
Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka makao makuu ya jeshi la polisi jijini Dar es salaam, kitengo cha polisi jamii, mrakibu mwandamizi wa polisi, Modestus Chambu, amesema polisi wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa pamoja na kuzingatia misingi ya haki za binadamu.
Akifunga mafunzo hayo ya siku moja, afisa mnadhimu wa polisi mkoa humo, kamishina msaidizi wa polisi Japhet Lusingu, akawahimiza maofisa hao kufikisha ujumbe kwa askari ambao hawakuhudhuria mafunzo hayo ili kuhakikisha zoezi zima la siku ya uchaguzi linamalizika kwa amani.