Alhamisi , 1st Oct , 2015

Asilimia 97 ya zahanati za serikali nchini zinadaiwa kuwa hazina maabara hatua inayosababisha makundi ya akina mama wajawazito, watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 na wazee kupoteza maisha hasa sehemu za vijijini.

Mwakilishi wa Katibu mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii Dkt. Hajas Senkoro

Akizungumza katika kongamano la kimataifa lililoshirikisha nchi mbalimbali za Ulaya, Asia na Afrika Mashariki kiongozi mkuu wa sayansi ya maabara nchini John Nyika amesema utafiti uliofanywa katika maeneo mbalimbali nchini umebaini kuwa ni asilimia 3 tu ya zahanati ndiyo zenye maabara.

Amesema hatua hiyo imesababisha jitihada za kitaifa za utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa kushindwa kufikiwa.

Akijibu changamoto hiyo mwakilishi wa katibu mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hajas Senkoro amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kubainisha kuwa serikali imeanza mchakato wa kuwasomesha wataalam wa sayansi ya maabara nchini kuanzia ngazi ya cheti ili waweze kusambazwa katika maeneo tofauti nchini.

Aidha ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya ujenzi wa maabara za kisasa inaendelea kufanywa ili kuweza kuboresha maabara nyingi nchini na kuondoa tatizo hilo la wananchi kukosa huduma ya maabaara kwa haraka.

Hata hivyo katika kongamano hilo baadhi ya wanasayansi wa maabara nchini walilalamikia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wataalam wa maabara nchini kwa kushindwa kutoa vipimo vilivyo sahihi kwa wagonjwa hatua ambayo Rais wa chama cha wanasayansi wa maabara nchini bwana Sabas Mrina kuahidi kufanya ukaguzi katika maabara zote za serikali na binafsi nchini ili kunusuru afya za wagonjwa.