Alhamisi , 27th Mar , 2014

Wafanyabiashara wa nchi za jirani huenda wakaacha kutumia bandari na ardhi ya Tanzania kusafirishia mizigo yao kutokana na kukithiri kwa wizi wa mizigo inaposafirishwa wakati ikiingia na kutoka nchini.

Tahadhari hiyo imetolewa na Msemaji wa Chama cha Wasafirishaji wa Malori TATOA Bw. Elias Lukumay ambaye amesema tatizo lililokithiri hivi sasa ni la wizi wa shaba inayopitia nchini wakati ikisafirishwa kwenda nje ya nchi na kwamba kwa wastani matukio sita hadi nane ya wizi wa shehena ya shaba hutokea kila wiki.

Lukumay amesema kufuatia hali hiyo, TATOA imekusudia kuwa suala la usalama wa mizigo ya wateja litakuwa moja ya ajenda kuu zitakazojadiliwa katika mkutano wake Mkuu wa mwaka utakaofanyika Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii.