Makamu wa Rais Dakta Mohamed Gharib Bilal
Akizungumza jijini Arusha kwenye mkutano wa kimataifa unaowahusisha wadau katika sekta ya manunuzi ya umma kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dakta Bilal amesema utaratibu mzuri katika eneo hilo utawezesha sekta hiyo sio tu kuvisaidia vyombo vyenye fedha na uwezo mkubwa, bali pia wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wadogo.
Makamu wa Rais amesisitiza kwamba lengo ni kuhakikisha mwananchi anapata manufaa ya jumla lakini pia kulinda mazingira, demokrasia na kuweka uwazi katika shughuli za manunuzi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake naibu katibu Mkuu wa jumuiya hiyo anayeshughulikia mipango na miundombinu Dkt Enock Bukuku akizungumza katika mkutano huo amesema uhuishaji wa sekta ya manunuzi kwa nchi wanachama kutaimarisha utekelezwaji wa itifaki nyngine zilizokwishasainiwa na zinazotarajiwa kusainiwa ikiwemo soko la pamoja, sarafu ya pamoja na hatimaye shirikisho..
Naye Afisa Mtendaji Mkuu mamlaka ya manunuzi ya umma Laurent Shirima amesema pamoja na ajenda ya kuhuisha mifumo ya manunuzi ndani ya Afrika Mashariki mkutano huo pia unaangazisha utaratibu wa matumizi ya mtandao ili kuweka uwazi na kupunguza malalamiko toka kwa wananchi.
Akiwa Jijini Arusha Makamu wa Rais pia amefungua mkutano wa kamati ya kudumu ya umoja wa nchi za Afrika unaolenga mkataba wa Afrika katika eneo la Demokrasia ya uchaguzi na utawala bora.
Katika Mkutano huo Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuridhiwa kwa mikataba ambayo nchi za Afrika zimeingia kwa kuhakikisha kunakuwepo na uchaguzi huru pamoja na kulinda haki za akina mama na watoto.