Alhamisi , 23rd Jul , 2015

Aliyekuwa mbunge wa Wawi Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Hamad Rashid amejiunga rasmi na chama chake kipya cha ADC leo na kukabidhiwa rasmi kadi ya uanachama.

Hamad Rashid Mohammed

Aliyekuwa mbunge wa Wawi Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Hamad Rashid amejiunga rasmi na chama chake kipya cha ADC leo na kukabidhiwa rasmi kadi ya uanachama.

Tukio hilo la kumkabidhi kadi limefanywa na mwenyekiti wa chama hicho Said Miraji katika mkutano maalum uliofanyika leo katika hotel ya Peecok jijini Dar es salaam, ambaye pamoja na nyaraka nyingine ikiwemo katiba ya chama, amesema kadi aliyokabidhiwa Hamad Rashid ni kadi namba moja ya chama hicho.

Naye Hamad Rashid pamoja na kukishukuru chama hicho kwa heshima kiliyompatia, amesema ameamua kujiunga na chama hicho kwa sababu ndicho chama pekee ambacho kinamtambua na kumtegemea mwenyezi Mungu katika sera zake na pia ni chama ambacho kinaamini katika vitendo zaidi kuliko maneno.

Katika hotuba yake , Hamad Rashid amesema kesi aliyokuwa ameifungua dhidi ya chama chake cha zamani cha CUF imekwisha baada ya yeye mwenyewe kuamua kuiondoa mahakamani, ili apate haki ya kugombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba na kwamba yuko tayari kulipa fidia ya gharama za uendeshaji wa kesi hiyo.

"Nimeambiwa kuwa gharama za kesi ziko palepale kwahiyo tutawalipa, lakini na wao watatulipa maana bado kuna ile kesi ya kututukana, kwahiyo tunalipa na wao wanalipa zaidi inakuwa ngoma drooo, maana walitaka kesi hii iendelee ili waje kuniwekea pingamizi wakati wa kugombea"

Aidha, amewataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi nchi nzima, hususan Zanzibar ambako Chama cha Mapinduzi kimekaa kwa zaidi ya miaka 50 bila maendeleo.

Akizungumzia demokrasia ndani ya vyama Hamad Rashid amesema vyama vingine vya upinzani haviwaandai watu wengine kushika nyazifa mbalimbali tofauti na ilivyo ADC, hivyo ni vyema watu wapewe nafasi badala ya kila mwaka mgombea kuwa huyohuyo.

“Haiwezekani kila mwaka anagombea mtu mmoja, ina maana hakuna wengine, vyama vyetu vina kasoro kubwa sana na kutowaandaa watu wengine kushika nafasi mbalimbali” Amesema Hamad.