Jumatatu , 4th Mei , 2015

Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya maendeleo ya jamii Saidi Mtanda, amemtaka waziri wa kazi na ajira Gaudensia Kabaka kukutana mara moja na viongozi wa madereva kwa lengo la kumaliza mgomo wa madereva nchi nzima ulioanza leo.

Mabasi katika kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kama yanavyoonekana pichani kufuatia mgomo wa madeereva nchi nzima.

Akizungumza katika mahojiano na East Africa Televisheni, Mh. Mtanda amesema mgomo huo umeathiri maisha ya watanzania wengi wasio na uwezo ambao wanategemea usafiri wa umma kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwa ni maisha yao ya kawaida.

Kwa mujibu wa Mtanda, suala ka usafiri ni moja ya huduma za umma ambazo kamati yake haifurahishi kuona zikizorota na kwamba kamati ya huduma za jamii ipo tayari kukutana na madereva hao kwa lengo la kumaliza mgomo.

Wakati huohuo baadhi ya wafanyabiashara jijini Dar es salaam wameelezea athari za kiuchumi za mgomo wa madereva leo kwani wamelazima kutumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri huku pia wakikosa wateja kutokana na wateja wao kushindwa kufika katika biashara zao sababu ya mgomo huo.