Jumamosi , 4th Jul , 2015

Tanzania imetupwa nje ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) baada ya sare ya 1-1 na wenyeji wao Uganda Cranes katika mchezo mkali uliofanyika jioni ya leo katika dimba la Nakivubo, Kampala, Uganda.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania taifa stars wakipasha misuli kabla ya kuivaa Uganda Cranes.

Matokeo hayo yanamaanisha, Stars imetolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 4-1, baada ya awali kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa Raundi hiyo ya kwanza huko katika dimba la Aman visiwani Zanzibar wiki mbili zilizopita.

Dakika 45 za kwanza zilimalizika kukiwa hakuna timu iliyopata bao na kipindi cha pili na kipindi cha pili, John Bocco ‘Adebayor’ alianza kuifungia Tanzania kwa penalti dakika ya 53 kwa penalti.

Penalti hiyo ilitolewa baada ya beki wa Uganda kuunawa mpira uliopigwa na mshambuliaji wa Tanzania, Rashid Mandawa lakini baadaye Uganda walifanikiwa kupata bao la kusawazisha kunako dakika za lala salama na hivyo wanasonga mbele katika mbio za kuwania tiketi yakucheza fainali hizo za michuano hiyo ya CHAN itakayofanyika mwakani nchini Rwanda.

Matokeo haya ya sare baada ya vipigo vitano mfululizo kwa Stars yanakuja chini ya kocha mpya, Charles Boniface Mkwasa akisaidiana na kocha Hemed Morocco na mshauri wao wa kiufundi kocha Abdallah 'king' Kibadeni waliopata nafasi yakukiongoza kikosi hicho hivi karibuni kufuatia kufukuzwa kwa Mholanzi, Mart Nooij ambaye alifungashiwa virago baada ya kufungwa na Uganda mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa huko Zanzibar.

Kwa maoni ya mashabiki wengi waliotazama mtanange huo wameonesha kupata matumaini si tu kwa matokeo ya mchezo huo bali pia ari, nia na upambanaji wa kujituma kwa wachezaji wa Stars ambayo iliundwa na chipukizi wengi wenye uwezo mkubwa ambao walipambana kwa dakika zote tisini za mchezo huo japo maamuzi ya waamuzi kwa wakati fulani yalionekana kuwa kwa wenyeji nakukumbusha msemo wa 'mgeni njoo mwenyeji apone'

Yote kwa yote kikosi cha stars kilicheza kandanda safi na la kuelewana pamoja na mapungufu machache hasa katika safu ya ushambuliaji kitu ambacho makocha watakifanyia kazi kwa wakati hasa ikizingatiwa mchezo mwingine wa kimataifa utapigwa mwezi Septemba dhidi ya Nigeria kuwania tiketi ya kucheza fainali za kombe la mataifa ya Afrika CAN.

Mara baada ya mchezo huo kochaa mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema anashukuru vijana wake wamejitahidi kucheza vizuri, mchezo ulikua mzuri timu ilitengeneza nafasi chache na kuweza kutumia nafasi moja iliyopatikana.

Mkwasa amewaomba watanzania kuendelea kuwapa sapoti, wamekaa na timu kwa muda mfupi wa wiki moja tu lakini katika mchezo wa leo mabadiliko yameonekana, hivyo wanahitaji muda kidogo kuweza kukaa na vijana kwa muda mrefu ili kujenga timu bora.

Stars inatarajiwa kurejea Tanzania siku ya jumatatu mchana kwa usafiri wa shirika la ndege la Rwanda Air.

Taifa Stars: Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Haji Mngwali, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Frank Domayo,/Said Ndemla John Bocco, Rashid Mandawa/Salum Telela, Saimon Msuva/Ramadhan Singano.

The Cranes: James Alitho, Muzamiru Mutyaba, Brian Ochwo, Hassan Waswa, Denis Oola, Faruk Miya, John Shemazi/Robert Sentongo, Bakaki Shafik, Tekkwo Derick/Kizito Hezron/Kalanda Frank.