Baadhi ya wachezaji wa mchezo wa chess wakichuana jijini Dar es Salaam
Mdoe ambaye ni Masta Kandideti anayetambulika kimataifa amesema hayo mara baada ya kumalizika kwa michuano ya chess ya kila mwezi inayoandaliwa na klabu ya Dar gymkhana ambapo amesema mchezo huo unahitaji damu changa ili upige hatua zaidi badala yakutegemea wakongwe ambao kwasasa umri umewatupa mkono.
Aidha Mdoe amesema kuwa kwa sasa mchezo huo unachezwa sehemu chache na wachezaji sio wengi na pia waliopo wengi ni watu wazima ambao wengi wao siku si nyingi watashinwa kuendelea na mchezo huo katika michezo ya ushindani wakibaki kucheza kwakujifurahisha zaidi hivyo ni wajibu sasa kwa chama cha mchezo wa chess nchini TCA kuchukua hatua stahiki ili kuunusuru mchezo huo ambao bado haujawaingia vizuri watanzania wengi.
Mdoe amesema mchezo wa chess ni wakila mtu na si wa tabaka fulani la watu na kama tunahitaji kupata matokeo chanya katika michuano mbalimbali ni lazima kuwekeza kwa vijana wadogo hasa walioko mashuleni kwani wao ndio wanaweza kumudu mchezo huo hasa kutokana na mchezo wenyewe kuhitaji mahesabu na kufikiri kwa muda mrefu kutokana na mchezo huo kuchezwa wa dakika nyingi kati ya saa moja hadi masaa matano hivyo kuwawia vigumu watu wenye umri mkubwa kuweza kucheza kwa muda mrefu na kufanya vema.