Alhamisi , 29th Sep , 2022

Kikosi cha wachezaji 20 , Viongozi pamoja na Benchi la ufundi kimeondoka leo Jijini Dar es Salaam kuelekea Ruangwa mkoani Lindi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Namungo utakaochezwa siku ya Jumamosi Oktoba 1 katika uwanja wa Majaliwa.

Kikosi hicho cha Wana Kino Boys kimeondoka mapema leo kikiwa tayari kimefanya maandalizi ya kutosha kuwakabili Namungo ambapo itakuwa ugenini kwenye mchezo huo.

KMC FC chini ya Kocha Mkuu Thierry Hitimana inatambua ushindani wa mchezo huo na kwamba kila kitu kimekamilika tangu Timu ikiwa Jijini Dar es salaam wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo.

Katika msafara huo KMC FC imeacha wachezaji saba ambapo wote hawana changamoto yoyote na kwamba wataendelea kufanya mazoezi binafsi kulingana na programu ya Kocha Hitimana kwa ajili ya kujiandaa na mchezo mwingine unaokuja Oktoba saba dhidi ya Ruvu Shooting.

"Tunakwenda kwenye mechi yenye ushindani, lakini tumejipanga vizuri, tunawafahamu vizuri Namungo, licha ya ushindani kuwa mkubwa lakini kama Timu tunakwenda kwa tahadhari Ili kuhakikisha kwamba tunapata ushindi.

Kwa upande wa hali za wachezaji wote wameondoka wakiwa salama, wanahali  nzuri, wanamorali zaidi ya kutafuta ushindi kwenye mchezo huo muhimu, mashabiki na Watanzania wote ambao sikuzote wanaisapoti Timu ni jukumu la kila mmoja kuwaombea wachezaji afya njema ili kuhakikisha burudani ambayo wameonesha kwenye michezo minne iliyopita inaendelea dhidi ya Namungo.