Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu ya Azam Fc Zacharia Thabiti (pichani)akiwa katika studio za East Africa Radio kujadili masuala mbalimbali ya michezo.
Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu ya Azam Fc amesema hatozuia tafsiri za wachambuzi na wadau wa mpira nchini juu ya kauli yake aliyoitoa kwamba klabu ya Simba iliwafunga jana kutokana na kazi nzuri ya nje ya uwanja iliyomaliziwa kama ushahidi uwanjani.
Kauli ya Zacharia Thabit inaibuka ikiwa ni siku moja baada ya Azam kuvuliwa ubingwa wa Azam Sports Federation Cup kwa kipigo cha bao 2-0 dhidi ya Simba na kufuta ndoto za wana lambalamba hao kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
Katika ufafanuzi wake kupitia kipindi cha michezo cha Kipenga cha East Afria Radio kinachoruka kila siku ya jumatatu hadi ijumaa kuanzia saa 2 usiku,Zaka Zakazi amesema kila mmoja anaweza kutafsiri anavyoelewa lakini maana yake ni kwamba wao walikua dhaifu kuliko kawaida.
Kuhusu kauli yake kuhusu uchovu unaohusishwa na kuwashwa kwa AC,kuwa huenda ikawa sababu ya wachezaji wake kuchoka maradufu,ni hisia zake na hakumaanisha katika vyumba vya kubadilishia nguo kwenye uwanja wa Taifa,bali ni katika kambi yao.
Katika hatua nyingine,Zaka Zakazi amewataka mashabiki kuacha kumhukumu na kumtishia kiungo wao Frank Domayo kwa kumchezea rafu mbaya beki wa Simba Shomari Kapombe katika mchezo huo uliopelekea asimalize mcheo.
Amebainisha kwamba kilichotokea jana sio mchezo wa kiungwana,ingawa mara nyingi matukio kama haya sio mageni kwani hata misimu kadhaa iliyopita,Kapombe wakati yupo Azam alishachezewa madhami kama hayo na mchezaji wa Simba Mohamed Ibrahim lakini hakuna aliyepaza sauti kama ilivyo leo.

