Jumamosi , 26th Dec , 2015

Ligi kuu Tanzania bara imeendelea leo kwa michezo sita huku ikishuhudia mabingwa watetezi, timu ya Yanga ya Dar es salaam ikiendelea kuchanja mbunga kwa kuishushia Mbeya City kipigo kizito cha mabao 3-0.

Ligi kuu Tanzania bara imeendelea leo kwa michezo sita huku ikishuhudia mabingwa watetezi, timu ya Yanga ya Dar es salaam ikiendelea kuchana mbunga kwa kuishushia Mbeya City kipigo kizito cha mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa Dar es salaam.

Mabao ya Yanga yamefungwa na Amis Tambwe katika dakika za 37 na 65, huku bao la tatu likifungwa na kiungo wake Thaban kamusoko katika dakika ya 66.

Katika mchezo huo imeshuhudiwa beki wa Mbeya City Tumba Sued akitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuonesha mchezo mbaya kwa wachezaji wa Yanga.

Mjini Shinyanga katika dimba la CCM Kambarage, Simba imebanwa mbavu kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mwadui FC inayofundishwa na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Simba imelazimika kusawazisha bao dakika za mwisho za mchezo kwa bao la Brian Majwega baada ya Mwadui kutangulia kufunga katika kipindi cha pili cha mchezo kupitia kwa Nizar Khalfan.

Jijini Tanga, hali ya Coastal Union si nzuri baada ya kuchezea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Stand United.

Mabao ya Stand yamefungwa na Haruna Chanongo dakika ya 13, Hassan Banda dakika ya 44 na Frank Hamis dakika ya 55 huku Coastal wakipata bao moja kupitia kwa Absalom Chidiebele kwa mkwaju wa penati dakika ya 75.

Mkoani Morogoro Mtibwa Sugar imeifunga Mgambo JKT mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Manungu Turiani Morogoro.

Mabao ya Mtibwa yamefungwa Henry Joseph dakika ya 16, Said Bahanuzi Dakika ya 48 na Shiza Kichuya dakika ya 77.

Mkoani Mtwara katika dimba la Ngwanda Sijaona, Ndanda FC imechapwa mabao 3-1 na JKT Ruvu inayofundishwa na Abdallah Kibaden, huku Majimaji ikiendelea kuzamishwa kwa kupigwa mabao 2-0 na Tanzania Prisons.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo miwili, ambapo Azam itakuwa nyumbani kuikaribisha Kagera Sugar na African Sports itaifuata Toto African jijini Mwanza.