Alhamisi , 11th Dec , 2025

Tume ya Uchaguzi ya Uganda imelaani machafuko makali yaliyotokea wakati wa mkusanyiko wa kampeni ya mgombea urais Robert Kyagulanyi Ssentamu, anayejulikana kama Bobi Wine, katika mji wa Gulu kaskazini mwa nchi siku ya Jumamosi tarehe Desemba 6, 2025, na ikalielezea tukio hilo kama “la kusi

Tume ya Uchaguzi ya Uganda imelaani machafuko makali yaliyotokea wakati wa mkusanyiko wa kampeni ya mgombea urais Robert Kyagulanyi Ssentamu, anayejulikana kama Bobi Wine, katika mji wa Gulu kaskazini mwa nchi siku ya Jumamosi tarehe Desemba 6, 2025, na ikalielezea tukio hilo kama “la kusikitisha na lisilo na sababu.”

Bobi Wine, kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP), alishutumu serikali ya rais wa sasa Yoweri Museveni kwa kutumia vurugu ili kuwatawanya au kuwanyamazisha wafuasi wake kabla ya uchaguzi mkuu wa 2026. Alisema kuwa “makundi ya watu walioajiriwa yalishambulia wafuasi wetu, yakawapiga, yakaharibu vifaa vya sauti na kuiba mali, huku mmoja wa madereva wa kampeni akiwa bado hajitambui.”

Katika taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Byabakama Mugenyi Simon, siku ya Jumatatu 8/12, tume ilieleza masikitiko yake kuhusu tukio hilo, hasa baada ya mkutano mpana uliozikutanisha pande zote za wagombea wa urais na uongozi wa polisi ya Uganda siku chache kabla ya tukio, ambapo kulisisitizwa umuhimu wa kufanya kampeni za amani zinazoendana na sheria.

Taarifa hiyo ilisema kuwa kilichotokea Gulu kinapingana na makubaliano yaliyotolewa awali na kunahujumu uaminifu wa mchakato wa uchaguzi, ikionya kuwa vurugu zinatishia uwezo wa nchi kuandaa uchaguzi huru na wa haki.

Tume ya Uchaguzi iliitaka polisi ya Uganda kufungua uchunguzi kamili kuhusu mazingira ya tukio hilo na kuhakikisha wahusika wote wanawajibishwa kisheria. Pia ilizitaka vikosi vya usalama kuwa na ustahimilivu na kutumia “mbinu za kisheria na kibinadamu, zinazolingana na hali” wakati wa kutekeleza maagizo ya uchaguzi.

Uganda inatarajiwa kufanya uchaguzi wa rais mwaka 2026, ambapo Bobi Wine atawania kupitia chama cha Jukwaa la Umoja wa Kitaifa “National Unity Platform”, naye Rais Yoweri Museveni atagombea kupitia chama tawala cha “National Resistance Movement” (NRM)