Jumamosi , 7th Mei , 2016

Wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa kwa ngazi ya vilabu barani Afrika timu ya Yanga hii leo wamedhihirisha wao kweli ni wakimataifa baada ya kuidunga mabao 2-0 timu ya Sagrada Esperanca ya Angola katika uwanja wa Taifa.

Mfungaji wa goli la kwanza la Yanga Simon Msuva akiwania mpira na beki wa Esperanca.

Shukrani kwa, wafungaji wa mabao hayo, Simon Happygod Msuva dakika ya 74 na Matheo Antony Simon dakika za majeruhi baada ya dakika 90 kumalizika, na sasa Yanga itahitaji sare ya aina yoyote ama isifungwe goli zaidi ya moja katika mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kuingia kwenye hatua ya makundi.

Katika mchezo wa leo kocha wa Yanga, Mholanzi Hans Van Der Pluijm alilazimika kufanya mabadiliko kwa wachezaji wawili baada ya kuwakosa nyota wake muhimu Wazimbabwe Donald Ngoma na Thaban Kamusoko na hivyo kuwaanzisha kwa pamoja washambuliaji Malimi Busungu na Amissi Tambwe huku katika kiungo Salum Telela naye akiziba nafasi ya Thaban Kamusoko.

Kwa ujumla hali ya mchezo ilikuwa ya mashambulizi ya kushtukiza kwa kila timu hasa kipindi cha kwanza huku Yanga ikionekana kukosa nafasi nyingi kupitia kwa Malimi Busungu na Amis Tambwe nakufanya nusu ya kwanza ya mchezo huo timu zote kutoka uwanjani zikiwa hazijaona mlango wa mwenzake.

Kipindi cha pili ndipo Yanga ambao walifanya mabadiliko kadha walianza kuona mafanikio baada ya kufika dakika ya 74, kiungo wa pembeni Simon Msuva alipofanikiwa kuiandikia timu yake bao safi kwa kichwa cha kurukia [kuchupa kama mkizi] baada ya Mwashiuya kuingia na kupiga krosi safi yaa chini na Msuva kufunga kiustadi.

Na kunako dakika ya 90+1 Matheo Anthony anafanikiwa kuweka hai zaidi matumaini ya Yanga na kutengeneza unafuu wa mchezo wa marudio baada ya kuunasa mpira na kugeuka nao na kupiga shuti kali la kushtusha bila ya kutegemea na mpira ukamgusa Antonio Kasule na kutinga kimiani.