Kikosi cha timu ya soka ya Yanga ya jijini Dar es Salaam.
Uongozi wa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika klabu ya soka ya Yanga umesema safari hii umejipanga vizuri vema kuhakikisha unavunja mwiko wa kutolewa na timu za waarabu wa Afrika hasa za kutoka Misri ambazo mara kadhaa zimekuwa zikihitimisha safari za timu za Tanzania katika michuano mbalimbali kwa ngazi ya klabu na taifa.
Akizungumza kwa kujiamini mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu hiyo Jerry Muro amesema jeuri ya waarabu ama dawa ya kuwadhibiti wameipata kwanza safari hii wana kikosi bora zaidi ya kile ambacho waarabu hao walikutana nacho mnamo mwaka 2014 ambapo Yanga waliondoshwa na timu hiyo kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya timu hizo kila moja kufanikiwa kumfunga mwenzake bao 1-0 nyumani kwake.
Jerry amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kwaajili ya mchezo huo ambao wao wanauchukulia kama fainali na wa kisasi ikikumbukwa kuwa timu hiyo ya Al Ahly waliwahi kuwatoa Yanga mwaka 2014 katika hatua hiyo, hivyo Yanga safari hii wamejipanga vema kuhakikisha wanafuta jeuri hiyo ya waarabu.
Aidha Muro amesema wameangalia maandalizi thabiti waliyofanya na wakakiangalia kikosi chao cha sasa ambacho kimeundwa kimataifa basi wana hakika watafanya kile ambacho wamepanga na hata upande wa wachezaji wenyewe wamejiapiza kamwe hawatataka tena kuwa uchochoro kwa warabu hao hivyo kesho ni lazima wapate ushindi mkubwa utakao warahisishia kazi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa April 20 mwaka huu jijini Cairo Misri.
Sisi dawati la michezo hapa Eatv kwaniaba ya watanzania wote tunazitakia kila la kheri timu zetu zote Yanga na Azam ambao nao Jumapili hii watakuwa na kibarua dhidi ya Esperance ya Tunisia katika mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika utakaopigwa katika dimba la Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.