Alhamisi , 2nd Jun , 2016

Klabu ya Yanga umewataka wanachama wote waliochukua fomu za kugombea uchaguzi wa Klabu hiyo kupitia Shirikisho la Soka nchini TFF kufika kamati ya maadili ya klabu ya yanga ili kujadiliwa.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga Jerry Muro amesema, pamoja na waliochukua fomu kutakiwa katika kamati ya maadili lakini pia wamechukua hatua ya kuwasimamisha uongozi wanachama wote waliosikika kuhusika katika kuhujumu mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo.

Muro amesema, Klabu ya Yanga inaangalia zaidi watu gani wataisaidia klabu hiyo na watawashughulikia wale wote ambao watahusika na hujuma za kutaka kuharibu uchaguzi katika klabu hiyo.

Muro amesema, kila mwanachama hai wa Yanga anahaki ya kupiga au kupigiwa kura na kwa yeyote atakayetajwa kuhusika na vitendo vya rushwa jina lake litakatwa.

Kwa upande wa TFF wamesema, June 08 mwaka huu wanatarajia kutana kwa ajili ya kutoa tamko rasmi kuhusu mchakato wa Uchaguzi wa Klabu hiyo.

Afisa habari wa TFF Alfredy Lucas amesema, wanaendelea kufuatilia kwa karibu kabisa mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Yanga na matamko mbalimbali yanayotolewa.

Lucas amesema, wanachama na wadau wa soka hapa nchini wanatakiwa kuwa watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi wa klabu hiyo.

Waliochukua fomu za ugombea wa nafasi mbalimbali katika klabu ya Yanga kupitia TFF ni Aaron Nyandana Titus Osoro wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ na Omari Said kutoka Zanzibar wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.