Kikosi cha Yanga
Meneja wa Yanga Hafeedh Saleh amesema, msafara utakuwa wa awamu mbili ambapo kocha msaidizi Juma Mwambusi pamoja na viongozi wengine wa benchi la ufundi wataondoka hii leo huku kikosi hicho kamili cha wachezaji kikitarajiwa kuondoka usiku wa kuamkia hapo kesho huku kikiwaacha wachezaji wake wanne ambao wanamatatizo mbalimbali.
Hafeedh amesema, wachezaji ambao hawatakuwa katika masafara huo ni beki Vicent Bossou ambaye anakadi zinazomzuia kucheza mchezo huo, Mshambuliaji Geofrey Mwashiuya ambaye anasumbuliwa na jeraha la goti, Deus Kaseke ambaye pia ni majeruhi pampoja na Hassan Kessy ambaye yupo katika mgogoro wa kimkataba baina ya klabu yake ya zamani ya Simba dhidi ya klabu yake ya sasa ya Yanga.
Hafeedh amesema, anaamini kikosi kitakachotua dimbani siku ya jumanne kitafanya vizuri kwa ajili ya kujiwekea matumaini ya kusonga mbele kutokana na kocha wa timu hiyo kufanyia marekebisho mapungufu yote aliyoyaona katika michezo yote iliyomalizika.
Yanga ambayo inashikilia mkia ikiwa kundi A inakwenda nchini Ghana ikiwa na kumbukumbu ya kutoshana nguvu ya kufungana bao 1-1 na Medeama Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.





