Jumanne , 24th Feb , 2015

Timu ya Yanga inatarajia kuondoka kesho kuelekea nchini Botswana kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya marudiano ya kombe la Shirikisho dhidi ya wenyeji BDF ya nchini humo itakayofanyika Februari 27 mwaka huu.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa habari wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro amesema, msafara utaondoka na wachezaji 20, benchi la ufundi likiwa na watu saba pamoja na viongozi wanne wa Klabu hiyo huku msafara ukiongoza na Ayubu Nyenzi kutoka Shirikisho la Soka nchini TFF huku wakiongozana na mashabiki 50.

Muro amesema, katika msafara huo watawaacha wachezaji wanne wakiwa majeruhi ambao ni pamoja na Mbrazili, Andrey Coutinho, Nizar Khalfan, Edward Charles na Mlinda mlango namba tatu wa Klabu hiyo Alphonce Matogo.

Yanga wanahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili kusonga Mbele ambapo katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam, Yanga walishinda 2-0 ambapo ikivuka katika raundi hii watakutana na Zimbabwe au Kenya katika raundi inayofuata.