Ijumaa , 1st Apr , 2016

Hatimaye chama cha mchezo wa kuogelea nchini Tanzania TSA kimefanikiwa kukamilisha mipango ya safari kwa waogeleaji watatu wa Tanzania ambao watakwenda nchini Dubai kushiriki michuano ya kimataifa ya kuogelea itakayoanza April nne mwak huu.

Baadhi ya waogeleaji wa Tanzania wakichuana katika moja ya mashindano ya ndani.

Wachezaji watatu wa mchezo wa kuogelea wa Tanzania wanataraji kuondoka nchini hapo kesho kuelekea nchini Dubai ambako wanakwenda kushiriki michuano ya mchujo ya kuwania nafasi yakushiriki michuano ya kufuzu Olimpiki ya Rio Brazil.

Katibu mkuu wa chama cha mchezo wa kuogelea nchini Tanzania TSA Ramadhan Namkoveka amesema vijana hao wamejianda vema na kimsingi wako tayari kwa mashindano hayo ambayo hujulikana kama Dubai International Aquatic Competition.

Aidha Namkoveka amesema wanaimani kubwa na vijana hao ambao wataungana na mwezao aliyeko huko Dubai na kufanya vema katika mtihani huo na kuweza kuweka rekodi na muda mzuri wa kukimbia kwamujibu wa muda wa kimataifa.

Namkovema amesema ni vema kwa Watanzania kuelekeza duwa zao zote kwa timu hiyo ili iweze kufanya vema na kufuzu kwa michuano ya olimpiki ya Rio Brazil itakayoanza mapema mwezi wa nane mwaka huu.

Akimalizia Namkoveka amesema pamoja na nafasi hiyo ya mashindano hayo ya kiamtaifa ya Dubai lakini bado kuna nafasi ya mwisho ya wachezaji kusaka nafasi ya kufuzu yatakayofanyika mwezi wa Julai mwaka huu ambayo nayo wanaimani ya kupeleka waogeleaji wengine zaidi ili kuongeza nafasi ya washiriki katika michuano ya Rio kama wakifuzu.