Jumatano , 18th Mar , 2015

Kiungo wa timu ya Coastal Union, Godfrey Wambura amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Februari mwaka huu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Wambura amechaguliwa kuwa mchezaji bora baada ya jopo la makocha linalofanya majumuisho ya wachezaji bora wa kila mchezo, ambapo kiungo huyo ameweza kuwapiku wachezaji Saimon Msuva wa Yanga, Abasirim Chidiebere wa Stand United na Gideon Benson wa Ndanda FC.

Jopo maalum la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa mechi hizo ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.