Jumatano , 1st Jul , 2026

Ujumbe wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema kuhusu suala la ndoa baada ya Pastor Rose Shaboka kusema ana Degree 4 hivyo hawezi kuishia kupika na kufua.

Picha ya Godbless Lema

"Tatizo la zama hizi ni kwamba tunawasilisha ndoa kana kwamba ni gereza la ndoto, wakati ukweli ni kwamba ndoa bora ni mahali ambapo ndoto za pande zote mbili hukua. Lakini juu ya ndoto zote kuna ndoto moja kuu zaidi, kuishi kwa furaha, upendo, heshima na unyenyekevu"

"Kufua boxer au kupika ukiwa na degree nne si udhaifu, kama ambavyo elimu si kipimo cha ubora wa ndoa wala thamani ya mtu. Mambo haya yanaweza kuishi pamoja bila mgongano"

"Elimu haimfanyi mtu kuwa mkubwa kuliko huduma, na huduma haipunguzi hadhi ya mtu. Mtu anaweza kuwa na shahada nyingi, akaongoza na kubadilisha jamii, na bado akachagua vitendo vya upendo ndani ya ndoa. Hilo si kushushwa hadhi, ni uchaguzi wa upendo"

"Tatizo huanza pale majukumu ya kifamilia yanapoonekana kama adhabu badala ya kujitoa. Ndoa si mashindano ya vyeo au vyeti, bali ni safari ya kuulizana, Leo nitakufanyia nini ili maisha yetu yawe bora zaidi"

"Ndoto za mtu mmoja mmoja zina thamani, lakini ndoa yenye afya hujengwa pale ambapo “sisi” inakuwa kubwa kuliko “mimi”. Wakati mwingine mmoja huweza kuahirisha au kubadilisha ndoto yake kwa ajili ya familia, huo si udhaifu, ni ukomavu"

"Mwisho wa yote, ndoa haijengwi na degree wala cheo, bali na upendo, heshima, unyenyekevu na kujitoa. Hapo ndipo ndoto mbili zinapogeuka kuwa maisha bora ya pamoja. Mwanamke hapaswi kuzuiwa kukua katika elimu na maarifa, lakini pia anapaswa kuelewa kuwa ukuaji wake wa kweli huonekana zaidi pale anapolinda ndoa kwa unyenyekevu, busara na hekima kama ilivyo kwa mwanaume pia"

“Ndoto za mtu mmoja zinakuwa muhimu, lakini katika ndoa yenye hekima, ‘mimi’ hufa ili ‘sisi’ iishi kwa upendo, heshima na unyenyekevu.”

NB: Pengine My beloved Sisy Rose alikuwa na msingi mzuri kwenye hoja yake lakini pengine uwasilishaji wake tu ulipaswa kwenda mbele zaidi kwa unyenyekevu na maarifa. Maana ikieleweka juu juu ni hatari sana.