Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Deloitte Kanda ya Afrika Mashariki Bw. Joe Eshun.
Wakizungumza katika mjadala wa bajeti uliandaliwa na taasisi ya ukaguzi wa mahesabu na ushauri wa kiuchumi ya Deloitte jijini Dar es Salaam leo, wachumi hao akiwemo mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Humphrey Mosha wamesema kwa ujumla bajeti hiyo ni nzuri na inatekelezeka.
“Ukipitia kitaalamu bajeti hii utaona kuwa kiasi kikubwa kimeleekezwa kwenye miundombinu na hiyo siyo kitu kibaya....kinachotakiwa na ambacho hakipo katika bajeti hii ni namna ya kuachana na kilimo cha kutegemea mvua. Nilichotegemea kukiona ni mipango au ya ujenzi wa mabwawa ya maji kwa ajili ya kilimo,” amesema Profesa Mosha.
Ameongeza kuwa “Unapozungumzia uchumi wa viwanda ni sawa na kutembea mguu mmoja huku na mwingine kule....hapa nina maana kwamba wakati unazungumzia viwanda huwezi kuacha kuzungumzia pia kilimo....kwahiyo ukiangalia bajeti hii utaona sehemu kubwa ya pesa imeelekezwa kwenye miundombinu kitu ambacho siyo kibaya kwani kilimo kinahitaji miundombinu bora ya mawasiliano ya mazao na bidhaa za kilimo kwenda kwenye masoko,”
Hoja ya Profesa Mosha imeungwa mkono pia na Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Deloitte Kanda ya Afrika Mashariki Bw. Joe Eshun ambaye kwa upande wake amesema licha ya kilimo kutengewa asilimia tano, bado bajeti hiyo ni nzuri na itasaidia ujenzi wa viwanda kupitia ukuzaji wa sekta ya kilimo kwani kiasi kikubwa kilichotengwa kwenye miundombinu kitasaidia kufungua njia za kuelekea vijijini na mashambani ambako mazao ndiko yanakolimwa.
“Licha ya uzuri wake, bado kuna mambo nadhani yanahitajika kufanywa ili kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara kama vile suala la matumizi ya teknolojia katika kilimo....sasa hivi duniani linaongelewa suala la intaneti of things......yaani matumizi ya teknolojia katika kila nyanja ya maisha....tukiliweka suala la teknolojia katika kilimo utaona bado Tanzania ina nafasi ya kufanya vitu vingi kwa ajili ya matumizi ya teknolojia katika kilimo,” amesema Bw. Eshun.
Bw. Eshun ametolea mfano matumizi ya teknolojia katika umwagiliaji kwamba bado wabunifu nchini hawajatumika ipasavyo kuisaidia nchi kutumia teknolojia katika eneo la umwagiliaji kwa mfano kujua kaina ya ardhi, kiasi cha maji kinachohitajika, upatikanaji wa mbegu bora na aina ya mazao yanayopaswa kulimwa katika ardhi husika.
“Wakati wa mkutano wa World Economic Forum tumeona nchi jirani ya Rwanda wao wamepiga hatua katika matumizi ya teknolojia. Kwa mfano sasa hivi dunia inaangalia matumizi ya ndege zisizo na rubani katika kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao na hata katika shughuli za utafiti badala ya kutegemea matumizi ya maafisa ugani waende moja kwa moja kwenye eneo la kilimo,” hayo ni baadhi tu ya maeneo ambayo teknolojia inaweza kutumika katika kilimo na kuongeza mavuno.