Jumatatu , 11th Nov , 2024

Wafanyabiashara Soko la Kariakoo, wameiomba Serikali kuwaondoa raia wa kigeni ambao wamekuwa wakiuza bidhaa rejareja kwa bei ya chini hali inayopelekea raia wa nchini kukosa wateja.

Wafanyabiashara wadogo, Soko la Kariakoo

Wakiongea na EATV, wanasema kwa sasa hali imekuwa mbaya zaidi kwani wengine wamekuwa wakisimama nje ya maduka na kuchukua namba za wateja na kuwapeleka kwenye maduka yao.

"Kinachofanyika ni kwamba hawa raia wa kigeni wamekuwa wakinunua  bidhaa kwao kwa bei rahisi, sisi tunanunua kwa bei ghali mpaka mizigo ije kufika Tanzania mfano bidhaa ya kuuza shilingi 6,000/= wao wanauza shilingi 3,000/=, kwahiyo wateja wanaondoka kwetu wanakimbilia kwao", Abas Ahmed, Mfanyabiashara Karikoo.

"Kama wao wanataka kufanya biashara basi wafanye uwekezaji watuuzie sisi ambao tuna maduka lakini sio wao kuuza kwa wateja wa rejareja, sisi tukienda kwenye nchi nyingine hatuwezi kuruhusiwa kuuza kama wao", Kombo Khamis, Mfanyabiashara Kariakoo

"Wanatukimbizia wateja, mwisho wa siku tutafunga maduka kwa maana uchumi wetu unadidimia kila siku changamoto mpya zinaibuka, tunaomba waondolewe au watafutiwe eneo ambalo watakuwa wanauza bidhaa kwa jumla", Musley Mahamoud, Mfanyabiashara Kariakoo

Mtaalam wa maswala ya biashara, kutoka kitivo cha biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Omary Mbura anasema wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza wakatumia changamoto hiyo kama sehemu ya kuboresha huduma kwenye biashara zao ili waweze kupata wateja.
"Hii maana yake ushindani umeongezeka, kwahiyo wanatakiwa kuboresha huduma  zao  kwa walengwa wao, wajijengee uwezo katika kuhakikish tunaboresha hudma zetu, na tuwasikilize wateja wanataka nini zaidi na wapinzani wetu wanafanya ili angalau tuweze kufikia huduma wanazotoa", Prof. Omary Mbura, Mtaalam wa Biashara UDSM.

Kwa upande wake Katibu wa jumuiya ya wafanyabaisahara, mkoa wa Dar es Salaam, Riziki Ngaga, anaelezea hatua walizochukua kuhusu uwepo wa raia wa kigeni kuuza bidhaa rejareja.

"Tumeishauri Serikali iweze kutenganisha hawa wazawa waweze kufanya biashara ndogondogo na wageni waweze kufanya biashara zile ambazo hatuna uwezo nazo , kwa sababu hata sisi9 kwenye nchi za wenzetu, hatuna uwezo wa kufanya shughuli ndogondogo  kama wao wanavyofanya lakini pia balozi zao tulijaribu kufatilia kama wana taarifa zao wamesema hapana tunashauri uhamiaji wawafatilie hawa walikuja nchini kwa ajili ya shughuli gani?", Riziki Ngaga, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoa wa Dar es Salaam.