Mamlaka nchini Nigeria imetangaza jana Jumapili, Desemba 21, kuachiliwa huru kwa wanafunzi 130 waliotekwa nyara mnamo Novemba 21 na watu wenye silaha kutoka shule ya Kikatoliki katika Jimbo la Niger, kaskazini mwa taifa hilo.
Kuachiliwa kwao kunafuatia tukio la mapema mwezi huu la kuachiliwa kwa takriban wanafunzi wengine 100 waliotekwa nyara mwezi Novemba.
Ujumbe uliochapishwa katika mtandao wa X zamani Twitter kutoka kwa msemaji wa rais wa Nigeria uliambatana picha ya watoto waliokuwa wakitabasamu nyuma ya basi dogo ambao kulingana na Sunday Dare, Mshauri Maalum wa Rais anayeshughulikia Mawasiliano ya Umma na Mwelekeo kwa Rais Bola Tinubu ni miongoni mwa watoto 130 wa shule waliotekwa nyara usiku wa Novemba 21 kutoka kwenye bweni la Shule ya St. Mary's katika kijiji cha mbali cha Papiri, kaskazini mwa Nigeria.
Kulingana na chanzo cha Umoja wa Mataifa kilichonukuliwa na shirika la habari la AFP, watoto wa shule watahamishiwa Minna siku ya Jumatatu, mji mkuu wa Jimbo la Niger.
Kulingana na Chama cha Wakristo nchini Nigeria, wanafunzi 315 na wafanyakazi walitekwa nyara mnamo Novemba 21. Karibu 50 kati yao waliweza kuwatoroka watekaji wao muda mfupi baadaye.
Baada ya kuachiliwa kwa takriban wanafunzi 100 mnamo Desemba 7, watu wapatao 165 walikuwa bado hawajapatikana, kulingana na takwimu zilizotolewa na dayosisi ambayo Shule ya St. Mary's iko. Kwa upande wake, Rais wa Nigeria Bola Tinubu aliripoti kwamba watu 115 walikuwa wakishikiliwa na watekaji nyara hao.
Utambulisho wao bado haujafichuliwa, na maelezo ya kuachiliwa kwa watoto hao bado hayajawekwa wazi.

