Jumamosi , 3rd Oct , 2020

Ligi kuu Tanzania bara raundi ya tano inaendelea hii leo kwa michezo minne itakayochezwa katika viwanja tofauti nchini.

Msimu uliopita katika uwanja wa Mkapa Yanga SC waliifunga Coastal union bao 1-0

Mchezo wa mapema leo unachezwa Saa 8 Mchana uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ambapo timu zilizotoka daraja la kwanza msimu uliopita, Gwambina FC ya Misungwi Jijini Mwanza itakipiga na Ihefu FC ya Jijini Mbeya.

Huu ni mchezo wa kwanza timu hizi zinakutana katika michezo ya ligi kuu kwani timu zote huu ni msimu wao wa kwanza kucheza ligi kuu.

Wenyeji wa mchezo Gwambina hawajashinda mchezo hata mmoja, wamefungwa michezo mitatu na sare mchezo mmoja ambapo hadi sasa wana alama moja na wapo nafasi ya 17 kwenye msimamo.

Wakati Ihefu FC wamekusanya alama 3 mpaka sasa wapo nafasi ya 16 kwenye msimamo, katika michezo minne iliyopita wameshinda mchezo mmoja na wamefungwa michezo mitatu huku wakiwa wamefungwa mabao matano na wao wamefunga mabao mawili.

Jijini Mbeya katika uwanja wa Sokoine itapigwa Dabi ya Jijini humo ambapo Mbeya City watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons.

Kikosi cha Mbeya City chini ya kocha Amri Said kinaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi hakina alama hata moja kwani wamepoteza michezo yote minne, wamefungwa jumla ya mabao saba na wao hawajafunga bao hata moja.

Tayari kocha Amri Said yupo kwenye wakati mgumu kwani anaweza kuwa kocha wa kwanza kufukuzwa kazi msimu huu endapo kama hawatapata matokeo ya ushindi katika mchezo wa leo.

Katika michezo mitano ya mwisho timu hizi kukutana kila timu imeshinda mara mbili kukiwa na sare moja.

Msimu uliopita Mbeya City waliondoka na alama 4 kati ya 6 dhidi ya Prisons ambao walishinda mchezo mmoja na sare moja.

Kikosi cha Tanzania Prisons kimekusanya alama 4 katika michezo minne wakiwa nafasi 11 kwenye msimamo, wameshinda mchezo mmoja, sare mchezo mmoja na wamefungwa michezo miwili dhidi ya Azam FC na KMC.

Katika uwanja wa Majaliwa Mkoani Lindi timu ya Namungo FC ni wenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga.

Namungo wanarejea katika uwanja wao wa nyumbani baada ya kucheza michezo miwili ugenini dhidi ya Mbeya city na Tanzania prison ambako walifanikiwa kuondoka na alama tatu tu kwa kuifunga Mbeya City lakini walipoteza dhidi ya Prisons.

Mchezo wa mwisho katika uwanja wa Majaliwa, Namungo walipoteza kwa kufungwa na Polisi Tanzania bao 1-0.

Kikosi hicho kina alama 6 na kipo nafasi ya 8 kwenye msimamo, wanacheza dhidi ya Mwadui ambayo imetoka kushinda mchezo wake wa kwanza msimu huu kwa kuifunga Ihefu bao 2-0 .

Kabla ya ushindi huo kikosi hicho kilipoteza michezo mitatu ya ligi mfululizo Mwadui wapo nafasi ya kumi na tano na alama tatu.

Msimu uliopita timu hizi zilitoka sare katika michezo yote miwili mchezo uliochezwa lindi ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, wakati ule ambao ulichezwa Shinyanga timu hizo zilitoka suluhu.

Na mchezo wa mwisho leo unachezwa saa 1 Usiku uwanja wa Mkapa Jijini Dar es salaam, mabingwa wa zamani na mabingwa wa kihistoria wa Tanzania bara, Yanga watakuwa wenyeji wa Coatal Union ya Tanga.

Kwa sasa Kocha wa Yanga Zlatko Krmpotić yupo kwenye shinikizo kubwa licha ya timu hiyo kutopoteza mchezo hata mmoja mpaka sasa, wakiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo na alama 10 katika michezo minne.

Lakini mashabiki wa Yanga hawaridhiswi na kiwango cha uchezaji cha timu hiyo wakidai hawachezi soka la kuvutia na wanaamini kocha ndio tatizo.

Pia kikosi hicho kimekuwa na uhaba wa ufunngaji mabao licha ya kufanya usajili mkubwa wa washambuliaji lakini mpaka sasa katika michezo minne ya ligi wamefunga mabao manne tu.

Yanga wanakutana na Coastal ya kocha Juma Mgunda ambayo imetoka kushinda mchezo wake wa kwanza msimu huu wiki iliyopita ambapo waliifunga JKT Tanzania bao 1-0 ambalo pia lilikuwa bao lao la kwanza msimu huu.

Coastal wana alama nne wakiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, msimu uliopita katika uwanja wa Mkapa Yanga waliifunga Coastal bao 1-0.

Katika muendelezo wa michezo ya raundi ya tano siku ya jumapili michezo mitatu itapigwa kabla ya kukamilishwa kwake siku ya Jumatatu kwa mchezo mmoja .

Kesho Jumapili

Biashara United Vs Mtibwa Sugar

JKT Tanzania Vs Simba SC

Azam FC Vs Kagera Sugar

Jumatatu

KMC Vs Polisi Tanzani