
Kikosi cha Gwambina FC kimepata ushindi wa kwanza msimu huu baada ya Kuifunga Ihefu FC mabao 2-0
Mchezo wa mapema uliochezwa Saa 8 Mchana, ilishuhudiwa Gwambina FC wakipata ushindi wao wa kwanza wa ligi kuu baada ya kuinyuka Ihefu mabao 2-0. Mabao yote ya Gwambina yakifungwa na Meshack Abraham dakika ya 33 na 48, Gwambina wamepanda kwa nafasi moja kutoka nafasi ya 17 hadi ya 16 wakiwa na alama 4 wakati Ihefu wanasalia na alama zao 3 wakishuka kutoka nafasi ya 16 hadi ya 17.
Kikosi cha Mbeya City kimepata alama yake ya kwanza msimu huu baada ya kutoka suluhu na Tanzania Prisons katika mchezo wa raundi ya tano wa ligi kuu Tanzania bara mchezo uliochezwa katika dimba la Sokoine Jijini Mbeya.
Licha ya kupata alama hiyo moja bado kikosi cha Mbeya City kinaendelea kuburuza mkia kwenye msimamo wa ligi, Tanzania Prisons imefikisha alama 5 na wapo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi na sare ya leo ni ya pili msimu huu katika michezo mitano.
Mkoani Lindi katika uwanja wa Majaliwa, klabu ya Namungo FC imepoteza mchezo wa pili nyumbani msimu huu baada ya kufungwa bao 1-0 na Mwadui. Bao la Mwadui FC limefungwa na Ismail Ally dakika ya 7 ya mchezo.
Mwadui wanapata ushindi wa pili mfululizo, mchezo uliopita waliifunga Ihefu bao 2-0. Ushindi wa leo unakifanya kikosi cha Mwadui kupanda kwenye msimamo wa ligi kutoka nafasi ya 15 hadi ya 8 wakiishusha Namungo mpaka nafasi ya 9 wote wakiwa na alama 6 Mwadui wakikaa juu kwa faida ya magoli ya kufunga.
Mchezo wa mwisho hii leo unacheza muda huu uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam Yanga wanaminyana na Coastal Union ya Tanga mchezo ambao umeanza majira ya Saa 1 Usiku.
Katika muendelezo wa michezo ya raundi ya tano siku ya jumapili michezo mitatu itapigwa kabla ya kukamilishwa kwake siku ya Jumatatu kwa mchezo mmoja .
Kesho Jumapili
Biashara United Vs Mtibwa Sugar
JKT Tanzania Vs Simba SC
Azam FC Vs Kagera Sugar
Jumatatu
KMC Vs Polisi Tanzani