Jumatano , 21st Oct , 2015

Ligi kuu ya soka Tanzania bara inaendelea hii leo kwa michezo minne kuchezwa katika viwanja tofauti nchini, huku timu 8 zikishuka viwanjani.

Kiongozi muandamizi wa timu ya Toto African ambayo inakaribishwa na Yanga uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Kabuka Bejumula amesema, wanaamini watacheza kwa kutafuta pointi tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi.

Bejumula amesema, katika mechi zote saba walizocheza wamefungwa mchezo mmoja na Mtibwa Sugar na wameshinda mechi mbili na mechi nyingine wametoa sare hivyo wanahitajika kucheza kwa nguvu ili kuweza kuifunga Yanga kwani hawajaja kujaribu bali kuifunga Yanga.

Bejumula amesema, Yanga haipo katika kiwango kikubwa zaidi kwani wote wanacheza uwanjani na wana miguu miwili hivyo wanaamini kuibuka na pointi tatu mbele ya Yanga ni rahisi.

Michezo mingine inayotarajiwa kupigwa hii leo ni huko mjini Shinyanga ambapo Stand United watakuwa wenyeji wa Majimaji katika uwanja wa Kambarage huku wajelajela Tanzania Prisons wakiwakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na wagosi wa Kaya, Coastal Union wakipepetana na Kagera Sugar katika uwanja wa Mkwakani jijini Tanga.