Jumamosi , 26th Apr , 2014

Didier Kavumbagu, Amis Tambwe na Yusuph Ndikumana wameiongoza timu ya Taifa ya Burundi 'Intamba Mu Rugamba' kuifunga Taifa Stars katika mchezo wa maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano uliopigwa leo jijini DSM.

Nahodha wa Timu ya taifa ya Burundi ambaye pia anaichezea klabu ya Yanga ya DSM, Didier kavumbagu

Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, leo imeshindwa kutamba mbele ya Burundi 'Intamba Mu Rugamba' baada ya kuchapwa mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa katika dimba la Taifa DSM.

Mchezo huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar na umeshuhudiwa na kocha mpya wa timu hiyo Martinus Ignatius aliyetua nchini hivi karibuni kuanza kuinoa timu hiyo, lakini akiishuhudia mechi hiyo kama mtazamaji tu huku katika benchi akiwemo Salum Mayanga.
 
Magoli ya Burundi yamefungwa na Didier kavumbagu dakika ya 45 kipindi cha kwanza, Amisi Tambwe dakika ya 55 kabla ya Yusuf Ndikumana kufunga bao la mwisho dakika ya 60 kwa shuti kali akiwa karibu na katikati ya uwanja.
Katika hali ya kushangaza mashabiki waliohudhuria uwanjani hapo walijikuta wakiishangilia Burundi na kuizomea Taifa Stars kwa kuonesha kiwango duni.
 Taifa Stars imecheza mechi hiyo ikiwa inajiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki michuano ya kombe la mataifa barani Afrika.