Taifa Stars inashika nafasi ya pili kwenye kundi H nyuma ya Congo DRC yenye alama 9 ikiwa imecheza michezo mitatu sawa na idadi ya Stars iliyojikusanyia alama 4 iliyo nafasi ya pili. Timu ya taifa ya Tanzania imepoteza mchezo ugenini dhidi ya Congo DRC kwa goli 1-0, mchezo wa marudiano wa kufuzu michuano ya AFCON 2025 unatarajiwa kuchezwa Oktoba 15, 2024 Uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es salaam.
Timu ya taifa ya Tanzania imepoteza mchezo wa kufuzu kucheza michuano ya AFCON 2025 yanayotarajia kufanyika nchini Morocco dhidi ya Congo DRC mchezo uliochezwa uwanja wa Stade de Martyrs. Mchezo huo ulitamatika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa goli 1-0, kwenye mchezo ambao Stars ilicheza vizuri ugenini.
Mwalimu Hemed Morocco alitengeneza mpango kazi mzuri sambamba na kuchagua Wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao walitekeleza vizuri mpango wa Kocha kwa dakika zote 90 nchini Congo. Stars iliongozwa na Nahodha Mbwana Samatta ilishindwa kuzitumia nafasi ilizozipata kutipita kwa Clement Mzize na Samatta.
Mwalimu Sebastien Desabre alitumia vizuri kipindi cha mapumziko kwani Wenyeji waliingia kwa kasi dakika 45 ya kipindi cha pili na kufanikiwa kupata goli la uongozi na la pekee kwenye mchezo huo baada ya Clement Mzize kujifunga dakika 53 kutokana na mpira wa kichwa uliopigwa na Chancel Mbemba kumgonga na kumshinda Ali Salim aliyekaa golini kwa upande wa Taifa Stars.
Matokeo hayo yameifanya Stars kusalia katika nasafi yake ya pili ikiwa na alama 4, huku mchezo wa marudiano wa kufuzu mashindano ya AFCON yatakayofanyika Morocco 2025 ukitarajiwa kuchezwa siku ya Jumanne Oktoba 15 Uwanja wa Benjamini Mkapa Dar es salaam. Tanzania inahitaji matokeo ya ushindi ili kuweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa AFCON kutokana na aina ya Wapinzania waliopo kwenye kundi H.
Licha ya kupoteza ugenini dhidi ya Congo DRC bado matumaini kwa Taifa Stars kufuzu ni makubwa kwa sababu inamichezo miwili itayocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani, mchezo wa Oktoba 15 na ule dhidi ya Guinea baada ya hapo itamaliza michezo ya kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika mwaka 2025 kwa kucheza ugenini nyuambani kwa Ethiopia.
Mechi itakayochezwa Benjamin Mkapa dhidi ya Wapinzani wao wa jana ni muhimu kwa kikosi cha Kocha Hemed Morocco ambapo watahitaji kutokupoteza nyumbani ili Wafikishe alama tano kabla ya kucheza dhdi ya Guinea, kama Tanzania ikifanikiwa kutokupoteza mbele ya Congo DRC kisha kushinda mchezo utakaofuatia itakua imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kumaliza kwenye nafasi ya pili kwenye kundi H hivyo kujihakikishia kushiriki AFCON kwa mara ya pili Mfululizo.
Stars imefanikiwa kushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika mara tatu katika historia yake huku ikapambana kutafuta nafasi ya kushiriki kwa mtawalia baada ya kufanikiwa kucheza mashindano yaliyofanyika nchini Ivory Coast mwezi Januari 2024, na iliondoka na alama moja kwenye michuano hiyo.
Tanzania itaandaa mashindano ya AFCON ya 2027 kwa kushirikiana na nchi Majirani za Kenya, Uganda hivyo kushiriki mashindano ya 2025 ni muhimu ili kuwapatia Wachezaji Vijana uzoefu kabla ya kuhodhi mashindano hayo makubwa kwa mataifa ya bara la Afrika.