Jumapili , 25th Aug , 2019

Klabu ya Soka ya Simba imetolewa nje ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kutolewa na timu ya UD Songo kutoka Msumbiji, kwa kutoka sare ya bao 1 kwa 1 huku mechi ya awali wakitoa sare ya bila kufungana.

Mechi hiyo iliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, UD Songo ndiyo waliokuwa wa kwanza kufumania nyavu za Simba kupitia kwa nahodha wake Luis kunako dakika 14 ya mchezo.

Bao la Simba lilisawazishwa na Nahodha Erasto Nyoni kwa mkwaju wa penati, kunako dakika ya 86, na kupelekea mpaka mwisho wa mchezo huo Simba 1 na UD Songo 1.

Kwa matokeo hayo sasa timu pekee ambazo zimesalia kwenye michuano ya Kimataifa kwa upande wa Tanzania ni Yanga pamoja na Azam FC ambao jana waliibuka washindi kwenye mechi zao.