Alhamisi , 19th Jan , 2023

Uongozi wa klabu ya Simba umefikia makubaliano ya kumwajiri Ouanane Sellami (42), raia wa Tunisia kuwa kocha msaidizi kwa mkataba wa miaka miwili.

Sellami ni mapendekezo ya Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ambapo ataungana na Juma Mgunda kuongoza benchi la ufundi.

Sellami ana Shahada ya Uzamili ya Elimu ya Viungo ya Michezo kutoka Taasisi ya Superieur Education Sportive Sfax ya nchini Tunisia.

Sellami ni kocha mwenye uzoefu na ana Leseni B kutoka Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) na kabla ya kujiunga nasi Sellami alikuwa akiifundisha Timu ya Almadina ya Libya kwa mwaka 2022 na mwaka mmoja nyuma alikuwa akiinoa Gabesien inayoshiriki Ligi Daraja la pili Tunisia.

Ujio wa Sellami kikosini ni kuliongezea nguvu benchi la ufundi kwa ajili ya michuano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.