Beki Hassan Ramadhan 'kessy' akiwa katika mazoezi ya Yanga.
Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umekanusha kuwafanyia mtima nyongo watani zao Yanga ili isimtumie aliyekuwa beki wa kulia wa timu hiyo Hassan Kessy katika mchezo wa kombe la shirikisho dhidi ya timu ya Mo Bejaia ya Algeria uliopigwa usiku wa kuamkia hii leo na Yanga kuchapwa kwa bao 1-0 na wenyeji hao katika mji wa Bejaia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe amesema jeuri ya klabu ya Yanga na kujiita wao klabu ya wananchi na kujiona wanaweza kila kitu bila kufuata utaratibu ndiyo kitu kilichowaponza na kushindwa kumtumia beki huyo pamoja na wachezaji wengine wapya waliowasajili hivi karibuni.
Poppe amesema Yanga baada ya kuona mambo yamekuwa magumu CAF ndiyo wakaanza kutafuta suluhu kwa kuutafuta uongozi mda ambao si siku ya kazi na hivyo kukwama kitu ambacho baadae sasa wanakigeuza kama hujuma ya makusudi ama kubaniwa na klabu ya Simba jambo ambalo si sawa kwakuwa wao ndiyo walizembea kwakuona mambo yatakwenda kirahisi kama walivyozoea kuburuza katika michuano ya hapa nchini inayosimamiwa na TFF.
Aidha Poppe ambaye ni captain wa zamani wa jeshi la wananchi Tanzania JWTZ amewataka Yanga kuja kutubu na kuomba wawapatie barua hiyo kwa heshima zote tofauti na walivyofikiri mwanzoni na vinginevyo itabidi wasubiri mpaka mwezi Julai wakati masuala ya usajili yatakapokamilika kwa timu zote katika usajili wa ligi za ndani.
Akimalizia Poppe amesema aina hii ya uendeshaji wa mpira wa ndani kwa klabu kaa ya Yanga kama wasipobadilika wataendelea kukwama kimataifa na kuona kama wanaonewa kumbe mambo waliyokutana nayo hayafanyiki kienyeji kama walivyozoea na kwa mantiki hiyo kama wataendelea kukaidi basi watakosa huduma ya mchezaji huyo na wenzake katika mechi watakazocheza hivi karibuni kabla ya hiyo Julai.
Katika mchezo huo wa jana usiku kuamkia hii leo Yanga pia ilishindwa kuwatumia wachezaji wengine watatu wa ndani kwa sababu kama ya Kessy, wachezaji hao ni kipa Benno Kakolanya aliyesajiliwa kutoka maafande wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya, Juma Mahadhi kutoka wagosi wa kaya Coastal Union ya Tanga na Andrew Vicent kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.