Jumanne , 7th Apr , 2015

Simba wamefufua matumaini wa kutwaa Ubingwa wa Ligi kuu Soka Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar mechi iliyochezwa Uwabja wa Kambarage Mjini Shinyanga.

Simba sasa imefikisha Pointi 35 baada ya kucheza mechi 21 ikizidiwa pointi moja tu na mabingwa watetezi Azam FC wenye Pointi 36 lakini wamecheza mechi 18 huku Yanga wenye Pointi 40 katika mechi 19 wakiwa kileleni.

Katika mchezo huo uliomaliza dakika 45 za kwanza bila bao huku Simba wakipata nafasi za kufunga lakini bahati ilikuwa sio yao lakini katika kipindi cha pili Simba walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Ramadhani Singano Messi dakika ya 52.

Bao la Simba lilidumu kwa dakika 12 ambapo Mshambuliaji wa Kagera Sugar Rashid Mandawa akisawazisha bao hilo na kumfanya kufikisha mabao 10 sawa na Mshambuliaji wa Azam FC Didier Kavumbagu huku wote wakiwa nyuma ya Winga wa Yanga Sc Simon Msuva anayeongoza kwa mabao 11.

Ibrahim Ajibu aliifungia Simba bao la pili kwa Penati katika dakika ya 71 kufuatia Erick Kyaruzi kuunawa mpira kwenye eneo la hatari katika harakati za kuokoa.