Jumatatu , 5th Mei , 2014

Klabu ya Simba imekabidhi marekebisho ya katiba yake ambayo yamepitisha kipengele kinachofuta nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na kuruhusu kiongozi wa juu wa klabu hiyo aitwe Rais na Makamu wa Rais.

Katibu mkuu wa Simba SC Ezekiel Kamwaga

Klabu ya soka ya Simba hii leo imekua klabu ya kwanza kutimiza maagizo ya TFF ya kufanyia marekebisho katiba za vilabu na vyama vya soka, baada ya msajili wa vyama na vilabu vya michezo kuikabidhi katiba hiyo hii leo.

Katibu mkuu wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga amesema katiba hiyo imepitishwa baada ya wanachama wa klabu hiyo kupitisha vipengele vya kuwepo kwa kamati mbili za maadili na rufaa, huku pia baadhi ya vipengele vikibadilishwa ikiwemo idadi ya matawi katika kata moja ambayo sasa yatakua mawili na nafasi ya uongozi wa juu utakua ukijulikana kama Rais na makamu wa Rais badala ya mwenyekiti na makamu wake.

Aidha Kamwaga amesema kipengele kinachomzuia mtu kugombea uongozi kutokana na kuwahi kufungwa kwa makosa ya jinai kinabaki kama kilivyo, huku katika kamati ya utendaji kati ya nafasi 5 za wajumbe moja lazima iwe ya mwanamke.