Rais wa Klabu ya Simba Evans Aveva akitoa maelekezo kwa timu ya viongozi siku ya Simba Day.
Klabu ya soka ya wekundu wa Msimbazi Simba SC inatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam keshokutwa kwenda Morogoro kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, msimu ambao unataraji kuanzia Agosti 20, mwaka huu.
Na baada ya maandalizi mazuri ya takriban mwezi mzima, Simba imeialika klabu bingwa ya Kenya, Gor Mahia kwa ajili ya kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki katika maadhimisho ya Tamasha maalumu la klabu hiyo maarufu kama Tamasha la Simba Day,ambalo hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 8 mwezi Agosti.
Rais wa Simba, Evans Elieza Aveva amesema kwamba uongozi wa timu hiyo uliamua kuahirisha programu ya mazoezi iliyopangwa kuanza jana mjini Dar es Salaam kwa ajili ya kupisha sherehe za Sikukuu ya Eid El Fitri.
Tamasha la Simba Day ni tamasha ambalo hutumika na klabu hiyo kutambulisha kikosi kipya kwaajili ya msimu mpya wa michuano mbalimbali, kutambulisha jezi mpya zitakazotumiwa na klabu hiyo lakini pia pamoja na kucheza michezo ya kirafiki ikiwemo huo dhidi ya Gor Mahia ya Kenya na mingine ya viongozi na kikosi cha timu B pia katika tamsha hilo huwa kunatolewa tuzo mbalimbali kwa watu walioifanyia makubwa klabu hiyo kwa namna moja au nyingine.
Kwa mujibu wa Aveva amesema kuwa wachezaji wote wapya na wazamani waliosajiliwa na timu hiyo kwaajili ya msimu ujao watakwenda kambini mjini Morogoro tayari kwaajili ya kuanza kujifua wakiwa chini ya Kocha Mkuu mpya Mcameroon Joseph Marius Omog ambaye aliwasili nchini wiki iliyopita na kukabidhiwa rasmi mikoba ya Muingereza Dylan Kerr, aliyefukuzwa Januari, ambapo kocha huyo ameingia kandarasi ya miaka 2.
"Kila kitu kinakwenda vizuri na Mungu akijaalia baada ya Sikukuu kupita, timu itakwenda Morogoro na si Lushoto kama ilivyoandikwa na gazeti moja," amesema Aveva.
Wakati huo huo habari kutoka ndani ya wekundu hao wa Msimbazi Simba zinasema kuwa aliyekuwa kocha wa mpito wa klabu hiyo Mganda Jackson Mayanja baada ya kufutwa kazi kwa kocha Muingereza Dylan Kerr, inasemekana mara baada ya makubaliano kati yake na uongozi wa klabu hiyo na mazungumzo mafupi na kocha mpya Mcameroon Joseph Omog sasa kocha huyo anakuwa rasmi ni kocha msaidizi wa timu hiyo baada ya kusaini mkataba wa miaka 2.

