Jumatatu , 26th Jan , 2015

Hali ya Mchezaji wa Simba Emmanuel Okwi imeendelea kuimarika baada kugongwa kiwiko nyuma ya kichwa kwenye mishipa ya fahamu hali iliyopelekea mchezaji huyo kupoteza fahamu na kukimbizwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Katika taarifa yake, Daktari wa Klabu hiyo Yassin Gembe amesema, Okwi alipoteza fahamu katika kipindi cha pili cha mchezo dhidi ya timu ya Azam ambapo aligongana na Beki Agrey Morris ambapo alipoteza fahamu na kukimbizwa katika zahanati ndogo ya Uwanja wa Taifa ambapo alipata huduma ya kwanza na kuanza kurejewa na fahamu lakini ilibidi kukimbizwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

Gembe amesema, Okwi atakuwa katika mapumziko mpaka pale hali yake itakapoendelea kuwa nzuri kwa ajili ya kuanza mazoezi.

Katika mchezo huo Simba ilitoshana nguvu na Azam kwa kutoka sare ya bao 1-1 ambapo bao Simba lilifungwa na Emmanuel Okwi katika dakika ya 18 huku Kipre Tchetche akiisawazishia Azam katika dakika ya 57.

Katika mechi nyingine za Ligi kuu Tanzania Bara, Ruvu Shooting imeifunga Mtibwa goli 2-1 mechi iliyochezwa uwanja wa Mabatini, Mlandizi, mkoani Pwani, huku Kagera Sugar ikifungwa na Ndanda bao 2-1 uwanja wa CCM Kirumba, Mjini Mwanza, Coastal Union ikiwafunga wenyeji Stand United bao 1-0, JKT Ruvu ikitoa sare na Mgambo mechi iliyochezwa uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam na Mbeya City ikitoka sare ya bao 2-2 na Tanzania Prisons, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya