Alhamisi , 9th Apr , 2015

Timu ya Taifa ya Soka la wanawake, Twiga Stars kesho inashuka Dimbani kupambana na Timu ya Soka la wanawake ya nchini Zambia She- Polopolo katika mechi ya marudiano Uwanja wa Taifa jiji ni Dar es salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Nahodha wa Twiga Stars Sophia Mwasikili amesema, wanachoangalia katika mechi ya kesho ikiwa ni pamoja na kufunga ni kulinda goli.

Mwasikili amesema, mpira ni mchezo wa makosa na huwezi kucheza bila kukosea lakini wanachoamini wao wataweza kuongeza magoli ili waweze kusonga mbele.

Kwa upande wake, Kocha msaidizi wa Shepolopolo, Kape Saili amesema wamejiandaa kwa ajili ya kuweza kushinda mechi hiyo na anaamini lolote linaweza kutokea kama ni kushinda, kushindwa au kutoa sare kwani Mpira ni dakika 90.

Twiga Stars iliifunga Shepolopolo mabao 4-2 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Nkoloma jijini Lusaka nchini Zambia na endapo timu hiyo, chini ya kocha Rogasian Kaijage itashinda tena mechi ya nyumbani, basi itakuwa imefuzu kwa ajili ya fainali za Afrika mwaka huu zinazotarajiwa kufanyika Congo Brazzaville kuanzia Septemba 4-9.