Kikosi cha timu ya taifa ya vijana Serengeti Boys wakiwa katika mazoezi kabla ya kuwavaa Wamisri watoto.
Timu ya taifa ya soka ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Tanzania Serengeti Boys wao wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya vijana ya umri huo ya Misri katika mchezo mkali mno muda wote wa mchezo huo uliopigwa katika dimba la taifa jijni Dar es Salaam.
Serengeti Boys ambayo inayonolewa na makocha wazawa Bakar Shime na Sebastian Mkomwa wakishauriwa na Mdenmark Kim Poulsen, hii leo imeonyesha mchezo mzuri na wakuvutia kwa muda wote wa dakika 90 za mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi mwenye beji ya FIFA Israel Mujuni Nkongo.
Magoli ya Serengeti Boys ambayo ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao yalifungwa na wachezaji Ally Hussein na Cyprian Suleiman [Bocco] huku goli la kufutia machozi kwa Mapharaoh hao watoto kutoka Misri likifungwa na mchezaji Dylaa Wahed.
Kwa mujibu wa taarifa za shirikisho la soka nchini Tanzania TFF na jumanne ijayo timu hizo zinataraji kucheza tena mchezo wa marudiano wa kirafiki safari hii ukufanyika pia jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Azam Complex ulioko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam maeneo ya Chamazi Mbande.
Serengeti Boys inacheza michezo hiyo na The Pharaohs ikiwa ni sehemu ya maandalizi na kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi ya Shelisheli Juni – Julai mwaka huu ambapo fainali za mwisho za michuano hiyo ama kilele chake kitakuwa nchini Madagascar hapo mwakani.
Kwingineko ni Ngarambe za michuano ya ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL ambapo hii leo tumeshuhudia Coastal Union maarufu kama wagosi wa kaya kutoka jijini Tanga wakiendelea kuchungulia kaburi la kurejea ligi daraja la kwanza mara baada ya hii leo wakiwa ugenini katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kukubali kichapo kizito cha mabao 4-0 mbele ya wenyeji wao wagonga nyundi wa jiji la Mbeya Mbeya City.
Mbeya City imepata ushindi huo kupitia kwa magoli ya wachezaji Hassan Mwasapili, Salvatory Mkulula na Ditram Nchimbi.
Na huko mkoa Shinyanga wenyeji Matajili wa almas timu ya Mwadui FC wamekubali kichapo cha nyumbani cha mabao 2-1 kutoka kwa wakata miwa wa Manungu Morogoro timu ya Mtibwa Sugar katika mchezo ambao ulichezwa huku uwanja ukiwa umetota kwa maji kufuatia mvua kubwa kunyesha huko Shinyanga nakupelekea uwanja wa Mwadui Complex kujaa maji na kuteleza katika baadhi ya maeneo.
Na kwa matokeo hayo Mtibwa sasa inafikisha alama 42 na kukwea hadi nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu bara huku Mwadui eso kwakipigo hicho wamesalia na alama zao 34 katika nafasi ya 6.
Ligi hiyo inataraji kuendeleatena jumapili hii April 03 kwa michezo minne kuchezwa katika viwanja tofauti hapa nchini, michezo hiyo ni pamoja na ile ya viporo itakayovihusisha vilabu vinavyopigania ubingwa wa ligi hiyo timu za Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo watakaowakaribisha wakata miwa toka Bukoba timu ya Kagera Sugar katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo mwingine utapigwa katika uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani wakati maafande wa JKT Ruvu watakapo waalika katika uwanja huo timu ya wanakimanumanu African Sports kutoka jijini Tanga timu zote zikitafuta alama tatu zakujinasua kutoka katika mstari wa kushuka daraja zikiwa katika nafasi tatu za chini.
Nazo timu za Toto Africans ya Mwanza na Azam FC ya Dar es Salaam zitachuana vikali katika mchezo mgumu kabisa utakaochukua nafasi katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza, huku huko Mtwara katika dimba la Nangwanda Sijaona wenyeji wa uwanja huo timu ya Ndanda maarufu kama wanakuchele watawaalika maafande wasiotabirika timu ya Jeshi la Magereza kutoka jijini Mbeya Tanzania Prisons.